Wednesday, January 4, 2012

Taarifa kwa Umma na Vyombo vya Habari kuhusu urudishwaji wa huduma ya Usafiri wa Reli ya Kati

Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) una furaha kuwataarifu kuwa kuanzia leo Januari 04, 2012 imerejesha huduma zake katika reli ya kati . Ambapo treni 4 za mizigo zimepangwa kuanzia safari kutokea Mororgoro kwenda Tabora, 2 kati ya hizo zimeshaondoka Morogoro kati ya saa 7 na 9 usiku kuamkia leo wakati nyingine 2 zilitarajiwa kuondoka saa 2 na 5 asubuhi leo.
Wakati huo huo huduma ya usafiri wa treni ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma imepangwa kuanza tena hapo siku ya Jumamosi Januari 07, 2012 saa 11 jioni, na kwamba wananchi wote ambao wanapendelea kusafiri na treni hiyo wafike katika stesheni zilizokaribu yao kukata tiketi za safari kuanzia leo Jumatano Januari 04, 2012.

Uamuzi wa kuanza kutoa huduma unatokana na kukamilika kwa matengenezo ya reli katika maeneo mbalimbali ya reli ya kati kuanzia mkoani Dar es Salaam, Pwani na Dodoma na hasa maeneo ya Gulwe na Godegode mkoani Dodoma ambayo yaliathirika sana na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na Dodoma.

Wahandisi na mafundi wa TRL walikuwa wanafanya kazi za ukarabati maeneo husika saa 24 bila ya kujali mapumziko na hivyo kuwezesha kukamilika kwa kazi za ukarabati kwa wakati. Aidha ziara za viongozi wa ngazi za juu wa Wizara ya Uchukuzi akiwemo Waziri, Mhandisi Omari R. Nundu na Katibu Mkuu Mhandisi Omar A. Chambo ziliwapa motisha wa kukamilisha kazi ya ukarabati kwa wakati.

Huduma za usafiri na usafirishaji zilisimamishwa rasmi katika reli ya kati kuanzia Desemba 20 mwaka jana ambapo Uongozi wa TRL ulilazimika kukodi mabasi yapatayo 25 siku ya Desemba 21, 2011 kuwasafirisha abiria 1834 wa treni waliokuwa wamekwama Dodoma wakitokea Kigoma kutokana na eneo la reli ya kati ya Stesheni za Gulwe na Godegode mkoani Dodoma tuta lake kusombwa na mafuriko ya mvua zinazoendelea nchini.

Taarifa hii imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Mhandisi K.A.M.Kisamfu.


MIDLADJY MAEZ
MENEJA UHUSIANO - TRL
DAR ES SALAAM.
JANUARI 04, 2012



No comments:

Post a Comment